Na. Jamaldini Abuu.
Singida. Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Migilango kata ya Tulya halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida wameililia serikali na mashirika binafsi kujitokeza kuwasaidia kupata huduma ya maji tofauti na maji wanayoyapata hivi sasa kwa kugombania katika visima ambapo kuna muda hulazimika kutumia na wanyama aina ya fisi
Wananchi hao wamesema wamekuwa wakitumia saa nne za kutembea kwenda na kurudi kisimani ambako wakifika maji huchota kwa kusubiria na kugombania kutokana na foleni kuwa kubwa wakiamka saa nane usiku na kurudi nyumbani asubuhi, muda mwengine maji hayo huyakuta yamechafuliwa kwa kutapikiwa na fisi hivyo kushindwa kuyatumia maji hayo licha ya kutumia muda mwingi kuyapata wakati wa usiku
Wananchi hao wameeleza hayo walipozungumza na KAJEM Tv June 3, 2024 walipojitokeza katika hafla ya uzinduzi na makakabidhiano ya mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya sh246 milioni wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi 4,000
Kwa mujibu wa meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Iramba Mhandisi Ezra Mwacha kata ya Tulya yenye vijiji vitatu kikiwemo kijiji cha Migilangi haijawahi kupata mradi wowote wa maji kutoka serikalini wala kwa wafadhili tokea nchi ipate uhuru
“kata ya Tulya ni kati ya kata kame katika wilaya hii ambazo hazijawahi kuwa na mradi wowote wa maji tokea uhuru wa nchi hii, lakini leo hii tumepata neema ya wafadhili waliotujengea mradi huu utakaohudumia wananchi wa kijiji chote cha Migirango” alisema
Kwa upande wake Rehema Namanigwa mkazi wa kijiji hiko amesema maranyingi hutoka majira ya saa nane usiku kufata maji kisimani maji ambayo hutumia wao na wanyama aina ya fisi huku akisema kuna siku walichota maji na waliporudi nyumbani wakabaini maji yananuka walipoyaangalia wakakuta mabaki ya nyama yaliotokana na fisi kutapikia maji hayo kabla ya wao kwenda kuchota
“Tulipofika nyumbani tulikuta maji yananuka tulipoyaangalia tukakuta mapandepande ya nyama kumbe fisi aliyatapikia ikabidi tuyamwage, tunaenda kufata maji mbali, tunatumia maji machafu, sio salama” alisema Namanigwa
Nae Grace Yowel mkazi wa kijiji hiko amesema licha ya kutoka saa tisa alfajir nyumbani na kufika kisimani saa 11 umbali wa masaa mawili, wanapofika mara nyingi hugombana wao kwa wao kutokana na uhaba wa maji hayo
“Ukienda kisimani unaanza kugombana kwaajili ya maji, ukirudi unaambiwa muda wote ulikuwa unafanya kazi gani mnaanza kugombana kesi zinakuwa nyingi nyumbani”alisema
Mwenyekiti wa kijiji hiko George Philemon amekiri kupokea kesi nyingi za wanandoa zilizotokana na shida ya maji kijijini hapo akisema kuna kina mama hutoka saa nane usiku na kurudi nyumbani saa sita mchana huku akisema afya na uchumi kwa wananchi wake vimedhoofika kutokana na muda mwingi kutumika kutafuta maji kuliko shughuli nyingine za kimaendeleo
“Nimepokea kesi nyingi sana kwaajili ya ugomvi wa maji hasa wanandoa, pia kwenye uchumi ulishadhoofika kwasababu watu muda mwingi wanafata maji tu badala kwenda kuangalia kazi za maendeleo hata afya zilishadhoofika mana maji yanayotumika ni machafu” alisema
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo mkuu wa wilya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda amesema hali ya upatikanaji wa maji kwa wilaya ya Iramba wamefikia asilimia 75 huku vijiji takriban 14 vikitarajia kupata maji kutoka katika mradi wa maji wa ziwa Victoria ambao tayari umeshafika kata ya Shelui wilayani hapo
Aidha ameongeza kuwa bajeti ya RUWASA wilaya ya Iramba imetenga sh700 milioni kwaajili ya kutekeleza miradi ya maji kijiji cha Tulya na Doromoni hivyo mara baada ya mwaka mpya wa fedha kuanza vijiji vyote vya kata ya Tulya vitakuwa na miradi ya maji
Mradi uliozinduliwa hii leo umefadhiliwa na Poul Due Jensen//Groundfos Foundation kutoka nchini Denmark na kutekelezwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Water Gate Community Link kutoka Dar es Salam kwa kushirikiana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Singida unathamani ya zaidi ya sh246 milioni na ulianza kutekelezwa mnamo march 23, 20224
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Groundfos foundation Ngusa Breck amesema mradi huo umetekelezwa kwa ubora wa hali ya juu tofauti na miradi mingine na kuwataka wahusika kuutunza mradi huo kwani miradi mingine hufa ndani ya miaka miwili na kwamba mradi huo utanufaisha hata watu wa nje ya kijiji hiko
Nae Mtendaji mkuu wa Water Gate Community Link ambao ni watekelezaji wa mradi huo John Mudende amesema mpaka sasa wameshaweka lita 50,000 kwenye matenk na wamejenga vituo vinne vya usambazaji maji katika kijiji hiko na kuwataka wananchi wautunze mradi huo ambao ni wakwanza kutekelezwa katika kata yao tokea wapate uhuru
“Kuna muda wafadhili wetu wanapita kukagua miradi, itakuwa vizuri tukija baada miaka tukute maji yanatoka, chondechonde tuutunze mradi huu” alisema
Tags:
HABARI