80% YA WANANCHI KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA IFIKAPO 2034

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko amesema kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ni dhahiri kwamba lengo la 80% ya wananchi kutumia nishati hiyo litafikiwa ifikapo Mwaka 2034

Shamimu amesema hayo Agosti 15, 2025 wakati wa kutambulisha mradi wa kusambaza majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa jiko unaoratibiwa na REA na kutekelezwa na Mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited iliyoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo katika Mkoa wa Katavi

Msululu wa wananchi waliojitokeza kupata Mitungi ya Gesi inayotolewa kwa Ruzuku kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majimoto, Seltus Mwanampemba alisema tunayo haja ya kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwani matumizi ya gesi yanasaidia kuokoa gharama

Nae mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule hiyo Dakson Schula alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha shule hiyo kupata nishati safi ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi

Kwa upande wao wananchi walionufaika na majiko ya ruzuku wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kununua majiko walipongeza hatua inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha wanananchi wa kipato cha chini nao wanafikiwa na wanabadilishiwa maisha yao

Wananchi waliojitokeza wakijiandikisha kupata Mitungi ya Gesi inayotolewa kwa Ruzuku kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Akizungumza kuhusiana na zoezi hilo la usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku,
 Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Joseph Sambali alisema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na hilo linadhihirisha kuwa wanadhamira ya dhati kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ambazo sio safi na salama na kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi

Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatumia njia mbalimbali katika kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha wananchi ili kufikia lengo la 80% ya wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo Mwaka 2034.



Post a Comment

Previous Post Next Post