WAKAZI SINGIDA WAFURAHIA UWANJA MPYA WA SINGIDA BS, WAZIBEZA SIMBA, YANGA

Wakazi wa Singida mashabiki wa Singida Black Stars na wapenzi wa mpira wa miguu wameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa uwanja mpya wa Singida Black Stars uliozinduliwa rasmi na naibu Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma huku wakizinyooshea kidole klabu kongwe nchini za Simba na Yanga

Wakizungumza katika nyakati tofauti uwanjani hapo mara baada ya ufunguzi wamesema uzinduzi wa uwanja huo iwe somo kwa timu kubwa nchini kutokana na Singida kuwa timu changa lakini imeweza kujenga na kumiliki uwanja wake huku timu kubwa zimeshindwa kufanya hivyo licha ya ukongwe wake

Kwa mujibu wa mjumbe wa bodi ya Singida Black Stars ambaye pia ni mbunge wa Makete Festo Sanga amesema uzinduzi huo ni awamu ya kwanza (Phrase one) ambayo ni eneo la kuchezea lililokamilika kwa asilimia 100 huku awamu ya pili ikiwa ni ujenzi wa majukwaa ya watazamaji

Ametumia nafasi hiyo kuwaita wadau kuwaunga mkono na kuwekeza kwenye ujenzi unaondelea hususani majukwaa na maeneo mengine ili kufanikisha uwanja huo kuwa bora kama ambavyo umekusudiwa mara baada ya kukamilika kwake

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma amesema kujengwa kwa uwanja huo kunaonyesha nia ya dhati ya ukuaji wa klabu hio changa huku akiwataka Singida Black Stars kuhakikisha wanapata matokeo na sio kuziacha timu kubwa za simba na yanga pekee

Uwanja huo uliojengwa eneo la Mtipa katika Manispaa ya Singida mkoani hapa, umepewa jina la AIRTEL STADIUM na rasmi Singida Black Stars watahama kutoka kuutumia uwanja wa CCM LITI kama uwanja wake wa nyumbani na kuhamia kwenye uwanja wao huo mpya


Post a Comment

Previous Post Next Post