MWENGE WA UHURU WAPOKELEWA MKOA WA SHINYANGA, UKITOKEA TABORA, RC. MBONI MHITA AONGOZA MAPOKEZI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Agosti 3, 2025 ameongoza wananchi katika mapokezi rasmi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025, yaliyofanyika katika uwanja wa Kituo cha Mabasi Kagongwa, wilayani Kahama.
Mwenge huo umepokelewa kutoka mkoa wa Tabora, na utakimbizwa umbali wa kilometa 819.2 katika halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga, ambapo utakagua, kufungua na kuweka mawe ya msingi katika jumla ya miradi 44 yenye thamani ya Shilingi bilioni 17.3.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Mhita amewapongeza wananchi kwa kuendelea kushiriki kwa wingi katika shughuli za kitaifa akisisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru siyo tu ishara ya ukombozi bali pia ni chombo cha kuhamasisha maendeleo, mshikamano na uwajibikaji.

“Tutumie fursa hii kuonesha mshikamano wetu kama mkoa, na zaidi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi itakayoguswa na Mwenge huu kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Mhita.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri za Kahama, Msalala, Ushetu, Shinyanga DC, Shinyanga Manispaa na Kishapu, ambapo miradi mbalimbali ya afya, elimu, maji, kilimo na mazingira itakaguliwa na kuzinduliwa.

Aidha Mwenge umezindua rasmi mradi wa bajaji unaotekelezwa na Kikundi cha Madereva Bajaji Kagongwa, katika eneo la Kagongwa, Wilaya ya Kahama, mkoani humo

Mradi huo umetokana na mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, na umewezeshwa kwa msukumo mkubwa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa uzinduzi kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Ismail Ali Ussi alisema mradi huo ni mfano bora wa namna fedha za umma zinavyoweza kutumika kuwainua wananchi kiuchumi, hasa vijana.

“Tunapongeza Kikundi cha Madereva Bajaji Kagongwa kwa uthubutu na matumizi bora ya rasilimali hizi. Hii ni njia mojawapo ya kujenga taifa linalojitegemea,” alisema Ismail.

Kwa upande wake, Katibu wa kikundi hicho, Izibu Ramadhan, alieleza shukrani zake kwa serikali, akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ununuzi wa bajaji 10 zenye thamani ya Shilingi milioni 110.

“Bajaji hizi si tu zimewapatia ajira vijana wenzangu, bali pia zimeondoa adha ya usafiri kwa wananchi wa Kagongwa. Tunamshukuru sana Rais wetu kwa moyo wa kutujali,” alisema Izibu.
Mradi huo umeanzishwa kwa lengo la kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, kuongeza mapato kwenye kikundi hicho pamoja na kutatua changamoto ya usafiri katika kata ya kagongwa kutokana shughuli za kibinadamu katika kata hiyo kuongezeka kila kukicha na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wanufaika na jamii kwa ujumla.

Aidha, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amewataka wananchi wa Wilaya ya Kahama kuiishi kikamilifu kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 inayosema: “Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Amani na Utulivu”, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu Mwaka 2025 Kwa Amani na Utulivu".
Chanzo: @

shinyanga_rs





Post a Comment

Previous Post Next Post