Naibu meya wa manispaa ya singida Geofrey Mdama amewataka wananchi hasa wa mkoa wa Singida kumuunga mkono Rais Dr. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa mazingira na kuhakikisha wanapanda miti kadiri wawezavyo
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika zoezi la upandaji miti 800 katika shule za msingi na sekondari Unyianga zoezi linaloendeshwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya TAA kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu nchini (TFS)
"Tumuunge mwanamazingira namba Moja Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwasababu anapenda mazingira na anafanya kazi kubwa sana kuleta maendeleo kwenye nchi yetu"
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Taasisi isiyokuwa yaserikali ya TAA Suphian Juma Nkuwi amesema hii ni kutokana na mkoa wa Singida kujulikana duniani kwa miaka mingi kama eneo kame kutokana na ukataji miti kwasababh ya shughuli za kibinadamu
Amesema wao kama Taasisi wanaadhima ya kurejesha miti iliopotea kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kupitia kampeni yao ijulikanayo kama 'SINGIDA MPYA YA KIJANI INAWEZEKANA'
"Tumeamua leo kuja hapa kwenye shule ya sekondari Unyianga kupanda miti 300 lakini pia tutapanda miti 500 katika shule ya msingi Unyianga lengo ni kuhakikisha ile miti iliokatwa miingi tunairejesha" alisema Suphian
Licha ya miti mingi kupandwa nchini, idadi kubwa ya miti hufa kutokana na usimamizi duni na kupelekea miti hio kufa ikiwa midogo kutokana na ukosefu wa maji ama kuliwa na wanyama huku wanyama wengine wakiwa ni wafugwao licha ya uwepo wa sheria ndogondogo za utunzaji wa mazingira mpaka ngazi ya kijiji
Hassani Wongoyo ni mtendaji wa kata ya Unyianga, amesema wamejipanga vizuri kusimamia Sheria zilizopo na kuwahamasisha zaidi wananchi kushiriki kwa pamoja katika kuhakikisha mkoa wa Singida unakuwa wa KIJANI
Mwalimu Martin Mwamlima ni mkuu wa shule ya sekondari Unyianga na mwalimu Ruth John ni mwalimu mkuu shule ya msingi Unyianga ambao wao wameishukuru Taasisi ya TAA kwa kushirikiana na TFS kuwezesha zoezi hilo la upandaji miti katika shule zao wakisema ni jambo litakalosaidia shule hizo kuwa na hewa nzuri na mazingira ya kuvutia
"Tuwape pongezi sana kwa kulifanya hili kwa moyo lakini pia tunawaahidi tutaendelea kuitunza ili ilete faida katika maisha yetu ya kila siku, tunafanya hivyo tukitambua kuwa tunaboresha mazingira yetu ya nchi nzima hasa mkoa wetu wa Singida" alisema Mwl. Ruth
Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya msingi Unyianga Rehema Ezekia na Abdulhalim Mohamed wamesema miti hio wataitunza kwa ushirikiano kwa kuzingatia faida watakazozipata kutoka katika miti hio
"Miti inazuia mmomonyoko wa udongo, inaleta mvua, tunapata hewa safi lakini pia tunapumzika kwenye hii miti, sisi wanafunzi tunashukuru sana kwa kutuletea hii miti tunaahidi tutaitunza kwa umoja na kwa kwanguvu" alisema Abdulhalim
Kampeni ya Singida mpya ya KIJANI inawezekana inaendeshwa chini ya Taasisi isiyokuwa yaserikali ya TAA chini ya mkurugenzi mtendaji Suphian Juma Nkuwi ikiwa na lengo la kupanda miti takribani million moja kwa mwaka mmoja katika Taasisi zote za umma huku mpaka Sasa ikiwa imeshafanikisha kupanda miti isiyopungua elfu 5
Tags:
HABARI