MADIWANI ITIGI WALILIA GHARAMA KUPATA HUDUMA ZA AFYA

Madiwani wa halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wamelalamikia kuwepo kwa gharama tofauti za upatikanaji huduma za afya katika halmashauri hio huku wakisema kuna baadhi ya huduma ambazo hutozwa malipo ilhali zinatakiwa kutolewa bila malipo

Hayo yameibuka hii leo August 1,2024 katika maswali ya papo kwa papo katika baraza la madiwani la halmashauri hio ambapo madiwani hao kutoka kata tofauti tofauti wamesema wamepokea malalamiko mengi kutoka Kwa wananchi wao hasa wakiitaja huduma ya mama na mtoto na huduma ya HIV kutozwa fedha

Wajumbe wa baraza la madiwani la halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wakiendelea na baraza

Elizabeth Kidolezi ni diwani vitimaalum, amesema malalamiko hayo si mara ya kwanza kuyafikisha kwa mganga mkuu wa halmashauri na wao kama madiwani walishashuhudia kliniki tembezi zikitoza pesa kwa wananchi

"Hata kwenye kliniki tembezi tumefika mahali Ipalanyo tukakuta watu wanatozwa pesa tukaona sisi wenyewe, ushahidi upo mwenyekiti kama anahitaji atuone tutampa ushahidi kamili" alisema


Baadhi ya wajumbe wa baraza la madiwani la halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wakiendelea na baraza

Nae Said Yahaya diwani wa kata ya Rungwa amesema kwenye maeneo kama Sikonge gharama inayotozwa ni elfu 7 lakini kwenye halmashauri yao gharama inaenda mpaka elfu 40 kulingana na matibabu ya mgonjwa husika

"Tunataka tufahamu tunatumia sera tofauti na Sikonge au sisi tunasera yetu?, Sikonge wao wanalipa elfu 7 lakini sisi papokwapapo mgonjwa anaweza akalipa hata elfu 35, 25 au 40 kulingana na matibabu ya siku hio" alisema Said

Baadhi ya watumishi na wakuu wa idara wa halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wakiwa katiba baraza la madiwani la halmashauri hio (Picha na Jamaldini Abuu)

Na kisha kuibuka hoja ya gharama za kufanyiwa upasuaji katika vituo vya afya vya halmashauri hio na kuelezwa kuwa licha ya kuwa upasuaji unaofanyika ni huohuo lakini gharama zinazotozwa zimekuwa zikibadilika

Diwani wa vitimaalum kutoka Mitundu Rose Madumba amesema katika vituo vyao vitatu vya Itigi, Mitundu na Rungwa upasuaji unaofanyika umekuwa na viwango tofauti tofauti wengine wakitozwa elfu 70, wengi laki moja na wengine laki mbili

Jambo lililoungwa mkono na mwenyekiti wa halmashauri hio Husseni Simba aliyehoji kuwa kama ni kuchangia kuleta vifaa vya upasuaji vinavyopungua kwanini gharama zitofautiane wakati upasuaji unaofanyika ni uleule?

"Tunataka tuelewe kiwango cha mtu anayefanyiwa upasuaji kwenye vituo vile anatakiwa atoe shilingi ngapi mana haieleweki, wengine wanalipa elfu 70 wengine laki moja wengine laki mbili" alisema Rose

Mwenyekiti wa halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida Husseni Simba akihoji uwepo wa gharama tofauti tofauti za upasuaji unaofanyika katika halmashauri hio (Picha na Jamaldini Abuu)

Akijibu malalamiko hayo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Itigi Ayoub Kambi amesema kwa mujibu wa sera ya afya ya taifa huduma ya mama na mtoto pamoja na huduma ya HIV zinatakiwa zitolewe bila malipo na kwamba malalamiko hayo ameyachukia na kwenda kuyafatilia ili kama yapo yashughulikiwe kwa haraka na hatua kuchukuliwa

"Sera kwa kina mama upasuaji ni bure kama kuna ulipishwaji naombeni nilichukue nilifuatilie kwenye vituo vyangu vya afya ili tujue wanalipishaje na kwanini wanalipisha na kwanini zinatofautiana lakini mimi najua ni bure" alisema Kambi


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida Ayoub Kambi akijibu malalamiko ya uwepo wa gharama tofauti za upasuaji unaofanyika katika vituo vya afya katika halmashauri hio (Picha na Jamaldini Abuu)

Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa halmashauri hio Frederick Gaisha amesema utofauti wa gaharama unatokana na utofauti wa hadhi ya vituo vya kutolea huduma hio ya afya akisema kuna gharama ya lipa papo kwa papo na lipa kwa huduma kulingana na hadhi ya kituo au zahanati

"Kuna sera ya lipa kwa huduma na kituo cha afya kinatumia sera ya lipa kwa huduma na hii sio kwa halmashauri ya Itigi tu ambayo ni tofauti na lipa papokwapapo, lakini zahanati zetu zote mpaka sasa wanalipa papokwapapo ya sh10,000" alisema Gaisha

Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida Frederick Gaisha akizungumza katika baraza la madiwani akijibu malalamiko ya uwepo wa gharama tofauti tofauti za upatikanaji huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma hio katika halmashauri hio. (Picha na Jamaldini Abuu)

Post a Comment

Previous Post Next Post