WAFANYABIASHARA WA NYAMA SINGIDA WAFUNGA MABUCHA

Wafanyabiashara wa nyama mkoani Singida wamegoma kufungua mabucha kwa kile walichokisema kupanda kwa bei ya ng'ombe

Wakizungumza hii leo Julai 1, 2024 wamesema sababu kubwa ya kupanda kwa bei ya ng'ombe ni kutokana na uwepo wa waarabu kutoka Uturuki na Misri ambao wananunua wanyama kwa bei ya juu katika minada na kuchinja kisha kutoa sadaka ya nyama hali inayowafanya wao kupata ng'ombe kwa bei ya juu huku wateja wakiwa wachache


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa wauza nyama manispaa ya Singida Omary Mbaraka amesema uhitaji wa nyama mkoani Singida haupo kutokana na wananchi wengi kupewa nyama bure na waturuki na wamisri hata baada ya sikukuu ya Eid kuisha

Ameongeza kwa kusema kuwa watu hao wananunua nao ng'ombe katika minada huku wao (waarabu) wakinunua kwa bei ya bila kujali ukubwa, uzito wala ubora wa ng'ombe wanachizingatia ni ng'ombe awe na damu jambo linalowafanya wao kutopata faida katika biashara yao


"Tumeshapeleka malalamiko yetu katika ngazi zote, tumeshapeleka barua kwa mkuu wa mkoa, tumekaa na Shekh wa BAKWATA mkoa, tumezungumza na mkuu wa wilaya lakini kinachokuja kuonekana ni kuwawekea mazingira mazuri hawa waarabu ya kuchinja kwahy tukaona sasa hakuna uhitaji wa nyama ya kuuza mana watu wanapewa nyama ya bure nyingi"



Aidha ameongeza kuwa hawana kikomo cha mgomo huo ni mpaka pale watakapojiridhisha hali ya soko lao kuwa sawa la wao kufanya biashara na kupata faida

"Kama wao tukiwauliza kwa mkuu wa wilaya wanasema hatuna muda maalum wa kuacha kuchinja au kutoa sadaka na sisi tunaona wananchi wanapata nyama tunaona kama vile hatuna umuhimu kwa sasa wa hii biashara"



Kwa upande wake Mfanyabiashara wa nyama Richard Robert amesema waarabu hao wananunua ng'ombe kwa bei ya juu akisema ng'ombe mwenye thamani ya laki mbili wananunua mpaka laki nne bila kujali hali ya ng'ombe na kuwa wanafika katika minada yote

"Hawa waturuki wamevamia Singida wananunua ng'ombe kwa bei ya juu, ng'ombe wa laki mbili wananunua laki nne ilimradi watimize lengo lao maana yake wao wananunua minadani kote wanachinja wanawagawia watu" alisema

Deogratius Joseph amesema ng'ombe wanaochinjwa hawajapimwa na wanagawa bure kama sadaka na kusema kuwa jambo linalowafanya wao wakae na nyama mpaka siku 4 buchani kutokana na kutokuwepo kwa wateja

"Wapewe utaratibu kuwa kuchinja ni siku 3 ili hizi siku nyingine tufanye biashara" 




Rukia Juma ni mamalishe ambaye yeye amesema mgomo huo umempunguzia wateja kutokana kwamba anategemea nyama kuuza supu na kuuzia chakula ila kutokana na mgomo huo hajui atauza chakula na nini huku 

"Nimeandaa vitafunwa inamana wateja wangu hawanywi supu, itaniathiri kwasababu nategemea nyama niuze supu, niuzie chakula sasahivi sijui nitauzia nini" alisema Rukia

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe amesema kufuatia hali hiyo tayari  ameshakaa nao pamoja wauza nyama na uongozi wa wilaya pamoja na wale wanaochinja kwaajili ya sadaka na kukubaliana kufanya hivyo mara moja kwa mwaka 

Amesema wafanyabiashara hao hawana malalamiko na serikali bali ni wale wa wanaochinja mitaani kama ibada na kwamba wamekubaliana ibada  hio ifanyike pia nje ya manispaa ya Singida tofauti na inavyofanyika sasa 

"Tumeshakaa nao tumezungumza na kukubaliana na sasa wanakwenda kufungua Ila maelekezo ya serikali wote tuzingatie yale tuliokubaliana lakini pia wazingatie masharti ya sadaka ili iweze kukubaliwa"alisema



Post a Comment

Previous Post Next Post