WAKULIMA WAOMBA ELIMU ZAIDI MFUMO WA STAKAKABADHI GHARANI

Jamaldini Abuu, Singida.

Baadhi ya wakulima wa zao la dengu katika halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida wameiomba serikali kupitia vyama vya ushirikia kupatiwa elimu zaidi juu ya mfumo wa stakabadhi gharani unaotekelezwa katika uuzaji wa baadhi ya mazao likiwemo zao hilo kwa njia ya mnada tofauti na sasa elimu wanaipata kutoka kwa watu wasio sahihi ambao ni madalali 

Wakulima hao wamesema madalali ndio wanaofika zaidi vijijini na kuwapotosha kuhusu mfumo huo huku wakivutia kwao ili waweze kuwalangua mazao wakisema kuwa mara nyingi wanaambiwa wakipeleka mazao yao katika mfumo huo watadhulumiwa na huenda ikachukua hata miaka mitatu mpaka mpaka kuuza mazao yao
Baadhi ya wakulima wa zao la dengu wilayani Manyoni wakisafisha zao lao kwaajili ya kuuzwa kwa njia ya stakakabadhi gharani katika ghara kuu la Utemini Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida (Picha na Jamaldini Abuu)
Wakizungumza na KAJEM TV katika ghara la Utemini Itigi linalotumika kukusanya na kuuzia zao la dengu kwa njia ya stakabadhi gharani, wakulima hao wamesema madalali wanaopita mtaani wananunua kwa bei kati ya 1,300 mpaka 1,500 huku wasimamizi wa mfumo huo wakisema kwa minada mitatu iliofanyika mpaka sasa bei haijashuka chini ya 1,900

Halmashauri ya Itigi tayari imeshafanya minada mitatu ya zao la dengu kwa njia ya stakakabadhi gharani ndani ya mwaka huu huku kukiwa na ongezeko kubwa la wakulima kupeleka mazao yao kutoka Tani 90 mnada wa kwanza mpaka Tani 2,800 mnada wa watatu ambayo imefanyika ndani ya wiki tatu na mnada wa nne wa zao hilo ukitarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii huku katika minada yote hio mitatu bei ikiwa haijashuka chini ya 1,900
Dengu ikiwa tayari imeshauzwa na kuhifadhiwa katika ghara ikisubiri kusafirishwa (Picha na Jamaldini Abuu)
Fidelis Mtoka ni mkulima kutoka kijiji cha kazikazi kata ya Kitalaka katika halmashauri hio ya Itigi ambaye amesema yeye mpaka sasa bado hajapata elimu ya kutosha juu ya mfumo huo hivyo haulewi na amebaki na maswali mengi juu ya namna mfumo unaendeshwa na bei inapatikanaje katika mfumo huo

Fidelis amesema elimu wanayoipata mtaani ni kutoka kwa madalali na Baadhi ya wakulima wanawaamini sababu hawana ufahamu wa mfumo, madali  ambao wauponda mfumo na kuvutia kwao kisha wananunua dengu kwa bei ya 1,300  

“kwangu mimi bado mfumo sijauelewa vizuri, changamoto kubwa inayotupata sisi wakulima ni kuhusu suala la bei bado elimu haijatufikia kujua labda kwamfano kwenye hii stakabadhi gharani dengu inauzwa shilingi ngapi kwa kilo, habari zinazoenea kule ni habari za madalali na ni habari mbaya kwamba ukipeleka mzigo kwenye ghara unadhulumiwa, unaweza ukamaliza miaka mitatu hujapewa hela”

Ameiomba serikali kutoa elimu kwa wakulima hasa wale wa vijijini zaidi ili waelewe itachukua muda gani kupata hela mara baada ya kupeleka mizigo gharani na kusema wakulima wapo tayari kusafisha mazao yao na kupeleka gharani ila changamoto ni uelewa wa mfumo
Zao la dengu likipakiwa kwenye roli kwaajili ya kusafirishwa baada ya kuuzwa kwa njia ya stakakabadhi gharani (Picha na Jamaldini Abuu)
Maneno hayo ya fidelis yanaungwa mkono na Issa Abdallah ambaye naye ni mkulima, anasema siku ya kwanza alipoambiwa kuhusu Kupeleka mazao gharani alipingana nao sana sababu hakuwa na elimu wala uelewa wowote kuhusu mfumo ila baada ya kufatilia alielewa mfumo upoje na akajiunga na mfumo 

Anasema hakuamini kama mfumo huo utakuwa kama Ambavyo anaushuhudia kwasasa na licha kuishauri serikali iwafikie zaidi wakulima hasa waishio nje ya mji anawahamasisha wakulima wenzako kuwa mfumo huo utawasaidia Kuepukana na madalali wa mtaani wananonunua wanaonunua dengu kwa bei ya sh. 1,500 huku katika minada yote iliyofanyika bei haijashuka sh. 1,900

“Ninawahamasisha wakulima, kwa mfumo huu utawaepusha na kunyonywa na madalali huko mtaani, madalali kwasasa wananunua 1,500 au 1,400 lakini hapa masoko yote tumeuza 1,900 na zaidi na pesa zimetoka kwa Wakati hazijachelewa”

Mwanne Mrisho na Simon Ngwelu ni Miongoni mwa wakulima waliopokea mfumo huo kwa furaha akisema kuwa mtaani walikuwa wakilipwa kwa kusuasua tofauti na sasahivi wanalipwa kwa wakati na hela sahihi na kwamba zamani waliogopa kutumia mfumo huo wakidhani umekuja kuwadhulumu 

“Mara ya kwanza tulikuwa tukiuza mtaani walikuwa wanatukaba wengine wanatulipa hela sio Sahihi lakini kwa hapa tukileta tunalipwa hela ambayo ipo katika mfumo na itatulipa nawaambia wakulima wenzangu waendelee kuitikia huu wito” alisema Mwanne

Halmashauri ya Itigi ni moja kati ya halmashauri zinazolima kwa wingi zao la dengu kama ambavyo anathibitisha mwendesha ghara kuu kwa mfumo wa stakabadhi gharani halmashauri ya Itigi na Manyoni Remigeous Kailembo ambaye anasema kadiri siku zinavyozidi kwenda wakulima wanajitokeza zaidi kupeleka mazao yao gharani

Amesema licha muitikio kuendelea kuwa mkubwa wanakutana na changamoto ya usafi wa mazao akisema bado wakulima hawana elimu ya kutosha ya kuandaa mazao yao na kuwataka wakulima wasafishe mazao ili aweze kuitisha minada miwili kwa wiki tofauti na sasahivi wanatumia muda mwingi kusafisha mazao kabla ya kuitisha mnada

"Mnada wa kwanza tuliuza Tani 90 ndani ya wiki tatu mnada wa tatu juzi tumeuza Tani 2,800 ila bado wakulima hawana elimu ya namna ya kusafisha mazao yao tunakumbana na hio changamoto" alisema
Kwa upande wake mwenyekiti wa AMCOS Utemini Itigi Geofrey Yohana amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima kwa kutumia magari ambayo yanazunguka ndani ya kl. 20 huku akisema mfumo huo walianza kuutumia rasmi mwaka jana bila mafanikio kutokana na muitikio kuwa mdogo sababu ya wakulima kutokuwa na elimu

Nae makamo mwenyekiti wa halmashauri ya Itigi Jonathan Dulle amesema kama halmashauri mpaka sasa wameshakusanya zaidi ya milioni 160 katika minada mitatu ambayo imeshafanyika kwa mwaka huu na kuwa mpaka sasa hawajapokea malalamiko ya mkulima yoyote kutopokea hela ndani ya masaa 48 mara baada ya mnada kufanyika kama ambavyo muongozo unavyotaka

"Pamoja na changamoto nyingine zote ambazo naimani zitakwenda kurekebishwa, lakini kupitia mfumo huu tulionao sasa sisi Maka halmashauri ya Itigi kupitia minada hii mitatu iliyofanyika tayari tumekusanya zaidi ya milioni 160 na hatujapokea malalamiko yoyote ya mtu kutopokea pesa ndani ya masaa 48 baada mnada kufanyika kama ambavyo muongozo unavyosema" amesema Jonathan

Post a Comment

Previous Post Next Post