EACOP YAZINDUA MPANGO WA MSAIDIE BINTI ABAKI SHULE

Kampuni inayotekeleza ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) imezindua mpango wa ‘Msaidie Binti Abaki Shule’ unaolenga kuwawezesha wasichana hasa waishio vijijini kudumisha usafi, kujenga kujiamini pamoja na kuhudhuria masomo bila ya vikwazo vitokanavyo na hedhi

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo awamu ya kwanza Meneja Uwezeshaji na Uwajibikaji kwa Jamii Clare Haule amesema tafiti bado zinaonyesha asilimia 15 mpaka 20 ya wasichana hukosa masomo siku 1 mpaka 2 kila mwezi sababu ya hedhi kutokana na kukosa uwezo wa kupata vifaa stahiki ikiwepo taulo za kike

“Mpango unaenda kutekelezwa kwa awamu na hii ni awamu ya kwanza kwa mikoa 3 ya Dodoma, Singida na Shinyanga na kwa ujumla tunategemea kufikia watoto 4,596 katika shule 18 na kila mkoa ni shule 6” amesema Clare
Aidha ameongeza kwa kusema kuwa mradi wa EACOP unatekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kurejesha ustawi wa maisha ya wananchi walioguswa na mradi huo kama vile kilimo, ufugaji wa nyuki, pamoja na elimu ya ujasiriamali na biashara  

Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo amesema uzinduzi wa mpango huo ni malengo yaliyopo katika Dira ya Taifa 2050 ambayo imelenga kuweka usawa wa kijinsia na kuweka mahitaji muhimu kwa watoto 

“Kwa kusaidia usimamizi wa afya ya hedhi tunajenga msingi wa wanawake bora na wenye uwajibikaji kwa Taifa letu”
Dkt. Victorina amesema ipo haja ya kuwalinda wasichana ambao kesho ambao watakuwa wanawake wema wa Taifa hivyo ni lazima kuwahakikishia wanapata mazingira salama ya shule na waweze kusoma kwa bidii huku Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Singida Regina Yaghambe akisema mpango huo umekuja wakati muafaka kwani utapunguza wasichana kukosa masomo kila mwezi kutokana na hedhi

Wakizungumza kando ya tukio hilo wazazi waliohudhuria tukio hilo wamesema awali walikuwa wakilazimika kuwapatia matambala ya nguo zilizoisha watoto wao ili kujisitiri na hedhi huku wengine wakitumia majani ya mimea 

“Tunashukuru EACOP kwa kuzindua mpango huu wa wasichana hasa wale wanafunzi walioko shuleni tulikuwa na hasara ya kutohudhuria shuleni tulikuwa tunawapa vitambaa walikuwa wakinyanyapaa na wenzake lakini sasahivi tunashukuru EACOP” Alisema Faulina Sinde mkazi wa Igauli
Nao wanafunzi waliopatiwa taulo hizo wamesema kwasasa wameongezewa kujiamini na kusoma kwa bidii kutokana na mwanzoni kukosa uhuru kuhudhuria masomo wanapokuwa katika hedhi 

Edina Metusaeli mwanafunzi wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari Ntonge amesema vifaa hivyo walivyopatiwa vinaenda kuwawezesha kuhudhuria vipindi bila kukosa tofauti na zamani wengine wakikosa masomo 
MABINTI WA SHULE YA SEKONDARI NTONGE WAKIWA WAMEBEBA VIFURUSHI MAALUM VILIVYOGAWIWA CHINI YA MPANGO WA MSAIDIE BINTI ABAKI SHULE

Uzinduzi wa mpango huu wa ‘Msaidie Binti Abaki Shule’ umefanyika katika shule ya Igauli iliyopo katika kijiji hiko kata ya Ntonge halmashauri ya wilaya ya Singida huku ujenzi wa Bomba hilo kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani mkoani Tanga ukifikia asilimia 80  za utekelezaji wake.
NAIMA CHONDO, KATIBU TAWALA WILAYA YA SINGIDA KWANIABA YA MKUU WA WILAYA YA SINGIDA GODWIN GONDWE
CHRISTOPHER KIDUBO,  KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI WA HALMASHAURI.
DKT. VICTORINA LUDOVICK, MGANGA MKUU WA MKOA KWA NIABA YA MKUU WA MKOA WA SINGIDA HALIMA DENDEGO
REGINA YAGHAMBE KAIMU AFISA ELIMU MKOA WA SINGIDA

Post a Comment

Previous Post Next Post